Thursday, November 8, 2012

Je unajua Wanaume wanaweza kuwekwa Kiganjani


Kuna baadhi ya wanawake walioolewa ambao wamekuwa wakijiamini sana kwamba hawawezi kusalitiwa eti wakidai kuwa, wamewaweka waume zao viganjani.

Maneno haya yaweza kuwa si mageni masikioni mwako. Huenda ulishawahi kumsikia mwanamke akisema: ‘Mimi mume wangu hapindui kwangu, nimemuweka kiganjani na hawezi kunisaliti kwani nampa kila kitu’.
Maneno haya yana tafsiri nyingi. Anayesema haya inawezekana kajidanganya kwa kwenda kwa waganga na kapewa vilimbwata, hivyo anaamini vitamfanya mumewe asimsaliti.

Mwingine anaweza kusema maneno hayo akimaanisha kuwa, anampa mumewe mapenzi kinyume na maumbile wengine wanaita tigo hivyo hakuna kitu ambacho anaweza kukifuata nje. Hii inatokana na ulimbukeni wa baadhi ya wanawake kuwa, eti wanaume wengi wanatoka nje ya ndoa zao kufuata kitu hicho.

Labda nikuulize wewe mwanamke kwani hicho unachodai unampa wengine hawana? kama ni kinyume na  maumbule hata ukimpa wewe kama ni wa kutoka nje anaweza kutoka na kudhani labda tigo ya nje ni nzuri zaidi.   Kwani wanaotoka nje ya ndoa zao unadhani nini wanachokifuata ambacho wewe huna! usijidanganye na hatimaye ukamkosea Muumba wako bure.
Naomba niwaombe enyi wanawake mnapenda mchezo huo acheni kwani ni hatari kwa afya zenu na pia hata vitabu vya dini vinakataza mchezo huo. Hiyo si dawa ya kumfanya mumeo asitoke nje ya ndoa.

Leo ngoja niwape  mbinu chache za kuwaweka waume zenu kiganjani.

Mpe mumeo anachohitaji
Wanawake wengi wanashindwa kujua wao wanatofautiana  na wanaume kwa hisia na hata mawazo ya mapenzi. Wanaume wana mambo wanayoyapenda kutoka kwa wake zao hasa katika masuala ya mapenzi. Kwanza wanawake wajue wanaume wengi wana hisia za haraka za kufanya mapenzi kuliko wanawake.

Mwanaume alivyoumbwa ni kwamba akiona tu  mfano mwanamke umevaa kanga moja au umevaa night dress hiyo inatosha kusisimua. Wapo wanawake wanaowasisimua waume zao bila wao kujua. Mfano umevaa tu kanga moja au night dress ndani huna kitu. Kwako ni jambo la kawaida lakini kwa mwanaume sio la kawaida kwa kukuona hivyo tayari unakuwa umeamsha hisia zake. Ukimwona anakuja kutaka haki yake usidhani anakusumbua. Ujue tayari mwenzako alishafiria mbali zamani we huna habari.

Ni vyema ukawa mwangalifu kujua hisia za mwanaume huyo mumeo kama inawezekana mpe anachohitaji kwani usipofanya hivyo unamwathiri kisaikolojia na anaweza kufikiria nje. Wanawake wengi wa nje waliowaweka waume zenu kiganjani hiyo ndio mbinu wanayotumia. Akiwa na ahadi na mumeo atamkuta kanga moja au amevaa night dress na kila anachohiji atapewa haraka tena kwa madoido. Kwanini akitaka hayo hayo kwa mkewe hapewi je ana kosa gani anapofikiria nje?

Sasa nikuulize wewe  mwanamke umemsisimua mwenyewe kwa mwonekano wako unamnyima ya nini.

Mvutie mumeo kwa mwenekano wako
Mvuto ni muhimu sana kwa mwanaume. Wanaume wanapenda wanawake wanaowavutia kihisia. Niwaambie wanawake mlioolewa jueni kumvalia mumeo mavazi yanayomvutia.
Sio vibaya kama nilivyosema hapo juu  ukavaa kanga moja kama upo pamoja nae. Kama nilivyoeleza hapo juu mwanaume anasisimka kwa kuona. Kwanini avaliwe kanga moja na wanawake wa nje wakati wewe unaweza kuvaa.

Wanawake jueni hili mnapokuwa karibu na waume zenu jianchieni Kwa mfano hakuna ubaya wakati mumeo karudi kutoka kazini akiwa amechoka, wakati unampotengea chakula  ukavaa kanga moja  au night dress. Unaweza kuona hilo ni jambo dogo lakini kisaikolojia utakuwa umefanya jambo kubwa. Hapo hata kama atakuwa ameudhiwa kazini atasahau na kukuona wewe mpenzi wake.

Usafi panga vitu vyako vya chumbani vizuri
Jambo hili limekuwa lizizungumzwa sana hadi wengine wanasema mwanamke usafi. Kisaikolojia mpangalio wa  vitu ndani na hasa chumbani kama ni mbovu unaweza kuathiri hata tendo la ndoa. Kama chumba ni kichafu vitu havijapangwa vizuri kisaikolojia kunapunguza msisimko wa mapenzi na hata kumfanya mwenzako achukie kufanya na wewe tendo hilo ukadhani hakupendi.

Mwanamke tandika kitanda chako vizuri panga chumba chako tandika shuka nzuri. Siku hizi kuna shuka zina maneno ya mapenzi nunua hiyo uwe unatandika. Kisaikolojia utamfanya mpenzi wako avutiwe chumba chako na hata wewe mwenyewe. Mazingira mazuri yatamfanya asisimke haraka  kimapenzi anapokuwa na wewe na hata kuitamana nyumba yake na kurudi mapema nyumbani.

Jinsi chumba kilivyo rafu ndiyo wanasakolojia wanasema kunafanya ubongo uwe rafu hata kuchukia. Unaweza kumwona mwenzako anachukia kumbe ni kutokana na mpangilio mbovu wa chumba ndio sababu inayomfanya achukie.

Uwe msafi wa mwili
 Sio usafi wa chumba pekee unatosha pia na usafi wa mwili wako ni muhimu. Niwakumbushe wanawake hakuna kitu kinachowachukiza wanaume kama mwanamke mchafu. Asiyejipenda. Sio lazima ujirembe sana lakini jitahidi ukawa msafi. Oga vizuri paka mafuta au lotion yako jipulizie manukato kidogo yanayomvutia mumeo. Sio lazima utumie gharama kubwa usafi wa kawaida unatosha.

Nikwambie wanawake wa nje hawana zaidi ya hayo ni hayo hapo juu na mengine ndiyo wanayotumia kuwaweka waume zenu kiganjani. Usijaribu kwenda kwa mganga hakuna atakachokusaidia memeo atatoka kama wewe humsisimui, hupangi vitu vyako vizuri na pia kama unaendekeza uchafu ni rahisi mumeo kufikiria nje.

Kujiamini kwako iwe ni kwa sababu unajua ‘kumhendo’ mumeo kwa kumpa mapenzi ya kiwango cha juu, kumheshimu, mjali na kumpatia  mambo ya msingi ambayo anastahili kuyapata kutoka kwako. Ukifanya hivyo utaifanya roho yake imsute kila anapotaka kukusaliti.

Hiyo ndiyo iwe sababu ya wewe kujiamini na wala huna sababu ya kujinadi kwa wenzako. Tambua kuwa kuna wanaofikia hatua ya kuhatarisha maisha yao kwa kutoa ‘mtandao’ wakijua kuwa ni njia ya kuwashika waume zao kumbe wanajitafutia matatizo makubwa.

Wapo waliopoteza fedha zao nyingi kwa kwenda kwa waganga ili waume zao wasifurukute mbele zao lakini imekuwa kazi bure. Shituka leo, anza kutumia mbinu sahihi za kuishikilia ndoa yako na usijidanganye kwa kufanya mambo ambayo ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu.

Mwanamke aliyekamilika ni yule anayeuthamini mwili wake, sasa kwa nini leo hii ukubali ‘kumrukisha ukuta’ mumeo ili kumfanya asiende nje? Kwa nini utumie fedha zako kwenye kumtafutia limbwata mumeo wakati wewe mwenyewe ni limbwata tosha?

Leo inatosha niishie hapa  tutaendelea siku nyingine. cheers!

Monday, October 29, 2012

Je unajua ni hatari kumdadisi mpenzi wako alitembea na wangapi?


KATIKA mapenzi kuna mambo ambayo hayastahili kupewa muda wa kuyajadili. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mengine yanaweza kutibua furaha iliyopo na kuweza kupindisha maisha yenu.

Kwa kuthibitisha hilo, sikia kisa hiki. Jamaa mmoja aliyefahamika kwa jina la Rashid alibahatika kumpata mke mzuri sana aliyefahamika kwa jina la Wahida. Yaani mwanamke ambaye kila mwanaume akimuona ni lazima atamani kuwa naye.

Baada ya mwanaume huyo kumuoa, waliishi kwa muda mrefu sana na ndoa yao ilikuwa ikitawaliwa na furaha siku zote. Wakabahatika kupata watoto wawili. Hakika mwanamke huyo alikuwa mke kwa maana halisi ya mke.

Alikuwa akimheshimu sana mumewe na kumpatia kila aina ya furaha. Kwa kifupi ilikuwa ni ndoa ya kuigwa. Siku moja Rashid alikutana na rafiki yake wa muda mrefu sana.

Mazungumzo yao yalikuwa mengi lakini ikafika mahali yule rafiki akamuuliza Rashid kama ameshaoa. Rashid akajibu kuwa kamuoa msichana mmoja anayeitwa Wahida. Yule jamaa akashangaa kusikia Rashid kamuoa Wahida, mwanamke ambaye siku za nyuma alikuwa ni changudoa.

Rashid aliposikia kuwa Wahida alikuwa changudoa, ati akaumia sana na akaanza visa kwa mkewe na hatimaye wakaachana. Akaoa msichana mwingine dogodogo kutoka kijijini ambaye hajaguswa. Alichokiona kwenye ndoa yake hiyo ya pili alijuta hadi akamkumbuka Wahida.

Tunajifunza nini kwenye kisa hiki? Ni kwamba, unapokutana na mpenzi wako kwa mara ya kwanza kuna mambo ya msingi ambayo kiukweli unastahili kuyajua. Hapa namaanisha historia ya maisha yake. Unapotaka kujua historia ya maisha ya mpenzi wako siyo lazima kila kitu ujue. Mengine yaache abaki nayo kwani hata akikuambia hayawezi kukusaidia kiviiile.

Lipo hili swali la umeshwahi kutembea na wanaume/wanawake wangapi hadi leo? Hili si zuri kumuuliza mpenzi wako. Kwa nini nasema hivyo? Nina sababu mbili. Kwanza ni vigumu sana kupata jibu la kweli, yaani tarajia kudanganywa. Hapo unaweza hata kuambiwa hajawahi kuwa na mpenzi kumbe katika ukweli tangu ameyajua mapenzi, ametoka nao zaidi ya kumi.

Sababu nyingine ya kwa nini hustahili kuuliza swali hilo ni kwamba, inaweza kukufanya ukabadili mawazo yako na hata uhusiano wenu ukakomea hapo. Unaweza kukutana na msichana mzuri sana mwenye kila sifa nzuri na katika historia yake ya mapenzi anaweza kuwa ameshapita kwa wanaume kibao kiasi kwamba hata idadi amesahau.

Sasa kama utamuuliza na yeye akawa mkweli kwako kwa kukujibu kuwa, ni wengi kiasi kwamba hata idadi hakumbuki, utajisikiaje?

Hakika unaweza kujikuta unanyong’onyea na kushangaa hata ile hamu ya kuendelea kuwa naye inaisha licha ya kwamba hukustahili kuwa hivyo. Matokeo yake unaweza kumkosa mtu ambaye alistahili kuwa na wewe na mkaishi maisha ya raha mustarehe.

Kuwa na idadi kubwa ni tatizo?
Kuna mtaalam mmoja aliwahi kusema kuwa, katika maisha ya sasa hakuna mwanamke anayeolewa akiwa na usichana wake na kama wapo ni wachache sana. Akaeleza kuwa, msichana akishatolewa usichana wake hata akiwa ametembea na wanaume ishirini hana tofauti na yule aliyetembea na wawili tu.

Mtaalam huyo akasema, tena inawezekana aliyetembea na wengi akatulia kwenye ndoa yake kuliko yule aliyetembea na mmoja au hajaguswa kabisa. Hapo ndipo inapoonekana kwamba, kuwa na historia ya kwamba uliwahi kutoka kimapenzi na wanaume/wanawake wengi, hakuna madhara makubwa katika ndoa.

Ndiyo maana inashauriwa kulifutilia mbali swali la kutaka kujua idadi ya wapenzi aliyowahi kuwa nao huyo mpenzi wako au hata kuwajua kwa majina. Hii ni kwa sababu hata ukijua haitakusaidia chochote zaidi ya kukuchanganya na kukufanya ukose imani kwa mpenzi wako.

kama utakuwa umenufaika usiwe mchoyo mwambie na rafiki yako naye asome safu hii kupitia www.kishindoleo.blogspot.com

Makala hii kwa hisani ya mtandao wa Global Publishers

Sunday, October 28, 2012

Pete ya Uchumba si Ndoa, Je mwanamke unajua hiyo ni nini?




Rafiki zangu leo tutajifunza kitu kipya kabisa. Naamini utabadili namna ya kufikiri mara mada hii itapofika ukingoni. Nazungumzia kuhusu pete za uchumba. Hizi zimekuwa maarufu sana katika jamii yetu siku hizi.

Watu wanakutana disko, wiki mbili baadaye wanavalishana pete! Tayari ameshachumbiwa na amekuwa chini ya miliki ya mtu. Uko wapi usahihi wa pete za uchumba? Vijana wamechanganyikiwa kwelikweli! Wanataka pete tu!

Inawezekana wewe msichana unayesoma mada hii sasa hivi umevaa pete ya uchumba au pengine uko njiani kuvalishwa...vizuri! Lakini unaelewa nini kuhusu pete ya uchumba? Unautumiaje uchumba wako na mpenzi wako?

All About Love pekee ndiyo mahali utakapoweza kutolewa matongotongo kuhusu suala la pete. Nikuambie kitu? Usiniache please, twende pamoja tuone ukweli.

NI NINI HASA?
Linatokana na neno la Kiingereza linaloandikwa engagement ring lenye maana nyingine ya commitment ring. Kwa Kiswahili rahisi ni pete ya ahadi. Msichana kuvalishwa pete ya uchumba, maana yake amevalishwa alama ya ahadi.

Jambo moja unatakiwa kusafiri nalo hapa ni kwamba, ahadi inaweza kutekelezwa au isitekelezwe. 

KUHALALISHA PENZI
Awali kulikuwa hakuna kabisa utaratibu huu wa pete za uchumba. Mvulana akimpenda msichana, taratibu za kawaida zilifuatwa kwa maana ya posa na baadaye mahari kisha ndoa. Hizi ni tabia za Kimagharibi ambazo zimekuja hivi karibuni.

Utaratibu huu umepokelewa vibaya (hasa na wasichana), wengi wamekuwa na shauku sana pete. Imani yao ni kwamba ukivalishwa tu, basi ndoa inanukia. Akipata mpenzi, anamlazimisha amvalishe pete.

Kwani kazi basi?! Aaah wapi! Jamaa anakwenda zake kwa Sonara anatengeneza pete ya laki tatu anamvalisha baa! Tayari wachumba! Hakuna mzazi wala mjomba anayejua. Hapo sasa ndiyo kwenye ukichaa – mwanamke atajiachia vyovyote atakavyo kwa mwanaume huyo.

Wanaume nao wanashangilia. Tatizo si pete? Anakuvalisha halafu anakutumia kwa nafasi, akiridhika anakuacha tena wengine huchukua na pete zao kabisa, halafu anatafuta mwingine anamvalisha. Mchezo unaendelea.

UCHUMBA SI NDOA
Dada zangu wapendwa fumbukeni macho, uchumba si ndoa. Utakuta mwanamke amevalishwa pete ya uchumba, basi kishakuwa mke. Atakwenda kwa huyo mwanaume, atafanya usafi, atafua, atapika na penzi atatoa!
Mwanaume anaridhishwa na kila kitu. Hapo unakuwa huna jipya tena. Hata kama anakupenda kwa kiasi gani, hawezi kuwa na haraka ya ndoa, maana kila kitu anachotakiwa kupata mwanandoa unampa!

Ya nini ajisumbue? Ya nini aanze kufikiria mambo ya vikao? Presha za nini? Haoni sababu na wakati muda ukizidi kwenda, anaendelea kukuchoka na kutafuta mwingine anayejitambua na kumuoa. Una lipi jipya utakalomwonesha ndani ya ndoa wakati kila kitu tayari anakijua?
Mabinti muwe makini. Kwa bahati mbaya sana, siku hizi wanaume wanakimbia kuoa mapema, ukijirahisi kwa pete utazivaa sana, lakini si ile ya madhabahuni. Utatumika na kuachwa.

UCHUMBA HUVUNJIKA
Acha kujidanganya, uchumba si ndoa (ingawa zipo zinazovunjika kulingana na ilipofungwa). Usiamini kuwa mchumba wa mtu basi kazi imeisha. Bado tena kubwa sana. Usikubali akutumie anavyotaka kwa kigezo cha pete.

Utakuta msichana amejitunza kwa muda mrefu sana lakini akishavalishwa pete tu, basi yupo tayari kwa lolote. Acha kujidanganya ndugu yangu. Endelea kujifunza na yeye anapaswa aendelee kukuheshimu kwa sababu bado si mke wake.
Baadhi ya madhehebu ya dini hutangaza ndoa kwanza kwa waumini kabla ya kufunga kwa sababu wanataka kupata uhakika wa wanandoa watarajiwa. Hata kama kanisani wanajua, kesho bwana harusi akikataa ndoa, hakuna wa kumlazimisha.
Kikitokea kipingamizi kadhalika, ndoa haifungwi tena. Kuwa makini.

UKWELI KUHUSU PETE
Achana na pete za kuvalishana uchochoroni. Mnavalishana pete gesti au kwenye kumbi za starehe – siyo sawa. Pete sahihi ni ile ambayo msichana atavalishwa mbele ya wazazi wa pande zote mbili, tena mahari ikiwa imeshatolewa na tarehe ya ndoa inajulikana.

Huu ndiyo usahihi na hapo tutakubaliana na wewe kwamba umevalishwa pete ya uchumba na upo mbioni kuolewa. Je, ukifikia hatua hiyo ndiyo ujiachie kwa mchumba wako? La hasha! Tena hapo ndipo unapotakiwa kuonesha heshima zaidi.

Kwamba wewe ni mchumba wa mtu na wazazi wako wanafahamu. Kuonekana mkiwa pamoja uchochoroni si kiashiria kizuri.  Je Kuna mahali nimekuacha? Nakupenda sana.

Mwisho kabisa kama umefurahia na umejifunza kitu kupitia makala hii usiwe mchoyo mwambie na rafiki yako asome naye makala hii hapa kupitia  www.kishindoleo.blogspot.com  kwa njia hiyo utakuwa umemsaidia asije akaingia mtegoni.

Usiache kusoma ukurasa huu wa Mapenzi  kuna mengi mazuri yanayokuja siku za usoni

Chears!

Makala hii imeandikwa na Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani

Makala nzima ni kwa hisani ya mtandao wa Global Publishers

Thursday, October 25, 2012

Unajua Wanaume wanapenda kuoa Wanawake wa aina gani?

Habari za wiki hii mpenzi msomaji. Mimi namshukuru Mungu kwa kuweza kunikutanisha na nyinyi kupitia safu hii ambayo pamoja na mambo mengine nazungumzia juu ya mada mbalimbali ambazo zinagusa maisha yetu ya kila siku.
Wiki hii nitazungumazia juu ya aina ya wanawake ambao wanaume wengi hupendelea kuoa. 
Wanaume wengi wanapofikia hatua ya kuoa si kwamba wanakurupuka tu na kuoa mwanamke yeyote mwenye sura nzuri, bali huchukua muda wao mwingi kuchunguza mambo mengi juu ya wake ambao wanadhani kwamba wanaweza kuwa pamoja kwa kipindi chote cha maisha.
Wanawake wengi wanajisahau na kudhani kwamba kitu kinachoweza kuwafanya wakapata wachumba ni uzuri hivyo kupoteza muda wao kujichubua na kujiremba ili wawavutie wanaume bila kujua kwamba kuolewa ni zaidi ya uzuri.
Hali sasa hivi imebadilika ni tofauti na kipindi cha nyuma ambapo ukiwa na sura nzuri na umbo la kuvutia basi una asilimia 100 za kuolewa. 
Utafiti ambao nimeufanya unaonesha kwamba zaidi ya uzuri wa tabia na umbo, kuna kuna sifa nyingine za msingi ambazo mwanamke anatakiwa kuwa nazo ili aweze kuwa katika mazingira mazuri ya kupata mchumba wa kumuoa kiasi kwamba asipokuwa nazo ataishia kuchezewa tu lakini haitatokea mtu kumtakiwa kwamba anataka kumuoa.

 
MWEYE MAPENZI YA KWELI
Lengo kubwa la mwanaume kuoa ni kutaka kupata mapenzi ya kweli kutoka kwa mwanamke na ikiwezekana waweze kupata watotoa ambapo watoto mara ndio wamekuwa furaha ya ndoa. Wapo wanawake wengine ambao wanonesha wazi kutokuwa na mapenzi ya kweli bali wanakuwa na mapenzi ya kuzuga. Wanachotaka wao aidha kupata umaarufu tu kwamba yuko na mtu fulani ama kuweza kupata pesa alizonazo mwanaume lakini sio kwamba ana mapenzi ya dhati kutoka moyoni mwake. 
Mwanamke asiye na mapenzi ya dhati utamgundua tu, muda mwingi utamuona macho yake yako kwenye mfuko wa mwanaume. Akiona kwamba mfuko umetuna utaona anaonesha mapenzi ya hali ya juu lakini pindi hali inapokuwa kubwa mbaya kifedha mapenzi yanaanza kufifia.
Kwanini wanaume wanapenda wana wake wenye mapenzi ya dhati kutoka mioyoni mwao na si kutokana na fedha walizonazo? Hii inatokana na ukweli kwamba maisha  siku zote yanabadilika, kama waswahili wanavyosema, kuna kupanda na kushuka.
Sio kwamba kila siku utakuwa na maisha mazuri na kama itatokea hivyo basi ushukuru mungu.Hivyo basi mwanamke wa kuoa lazima afahamu hivyo na awe tayari kuonesha mapenzi yake ya dhati wakati wote wa maisha yao na si kwa kipindi fulani tu cha neema.
 
Si hivyo tu pia asilimia kubwa ya  maisha ya  ndoa yanatawaliwa na mapenzi, kwa hiyo nyanja hiyo inakuwa ya msingi sana kwa wanaume wengi kuiangalia  ili wasije wakajikuta wanaoa mwanamke ambaye baada ya muda mapenzi yanakwenda likizo hali ambayo inaweza kuwafanya wasiishi maisha ya raha mustarehe.
 
WENYE TABIA NZURI
Tabia njema ndio silaha ya maisha, ukiwa na tabia nzuri kila mtu atakupenda, hiyo ni katika maisha ya kawaida. Lakini linapokuja suala na kuoa tabia inakuwa kitu cha awali sana kungaliwa na hiyo inaweza kuwa na ukweli kwa sababu wapo wasichana wazuri wenye mvuto wa aina yake na maumbile mazuri, lakini  wanakosa wanaume wa kuwaoa, ukiuliza kwani utaambiwa  anatabia mbaya.
Naweza kusema hilo ndilo limekuwa tatizo kubwa kwa baadhi ya  wanawake kukosa wanaume wa kuwaona. Hakuna mwanaume hata mmoja kati ya wale ambao nimejaribu kuongea naye ambaye ameonesha kulidharau suala hilo la tabia.
Si hivyo tu wapo wanaume  ambao wameingia kichwa kichwa na kuoa kwa kuangalia sura tu bila kujali tabia, matokeo yake baada ya siku chache yanatokea machafuko ya aina yake hali ambayo imepelekea kuvunjika kwa ndoa kutokana na tabia mbaya alizonazo mwanamke.
 
WENYE UCHU NA MAENDELEO
 
Hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko ya aina yake kwa wanaume, wengi sasa hivi hawapendi kabisa kuoa mwanamke ambaye hana kazi yaani 'golikipa'. Kama atakuwa hana kazi basi awe na uchu wa maendeleo kwa kujituma kufanya kazi mbalimbali za kimaendeleo kama vile kilimo kwa wale walio vijijini na biashara ndogondogo kwa wale ambao wako mijijini na hata vijijini. 
Ile dhana ya kusema mwanamke ni mama wa nyumbani wa kukaa na kujipodoa akimsubiria mwnaume arudi amstarehesha, sasa hivi imepitwa na wakati. Wanaume wengi wanapenda wanawake ambao ni wahangaikaji, wenye ndoto za maendeleo katika maisha yao. Hata kama watakuwa si wafanyakazi lakini wawe wenye kutoa ushauri kwa waume zao juu ya jinsi gani wafanye ili wafanikiwe.
 
WASIOPENDA MAKUU
 
Kuna  wanawake wengine wanakuwa na tabia za ajabu sana kiasi kwamba yaweza kuwa kero kwa wanaume. Wapo wanawake ambao wanapenda makuu bila kujali hali halisi ilivyo. Kuna wanawake naweza kusema wana tamaa, kila wikiendi utamsikia "leo tunakwenda wapi dear?"
  
Akimuona rafiki yake kanunua simu ya laki tatu na yeye utamsikia akisema, ‘na mimi naomba uninunulie simu kama  ya Grace’. Ukienda naye Pub anakuambia, "mimi sinywi pombe za chupa natumia za kopo tena Heineken’. Yeye hajali kiasi cha pesa mwanaume alicho  nacho na usipotekelezea anachukia na anaweza hata kupunguza mapenzi.

 
Wanawake kama hawa wako katika mazingira magumu sana ya kuweza kupata wanaume wa  kuwaoa.  Mara nyingi katika maisha fedha huzungumza, kama mwanaume atakuwa na pesa ya kutosha itakuwa rahisi sana kwa mwanamke kupata kila atakachopenda lakini si kwa kumwambia mimi nataka kitu fulani.Mwanaune mwenyewe utamsikia akisema, ‘unataka nikununulie simu ya aina gani, au leo unataka twende wapi?’ hapo ndipo utakuwa na nafasi ya kusema, ‘mimi nataka uninunulie simu kama ya fulani ama leo nataka twende sehemu fulani.’
Wanaume ni warahisi sana wa kuwapatia wale ambao wanatarajia kuwaoa chochote ambacho watahitaji kama tu pesa haitakuwa  tatizo. Kitu ambacho kinawaudhi wanaume wengi  ni ile tabia ya mwanamke kupenda mambo makubwa bila kuangalia uwezo uliopo kwa mwanume.
Kuna wanawake wengine wao si wasemaji kabisa, yeye anasubiri leo amemletea hiki, anapokea na kushukuru, kesho akiambiwa twende beach anakubali. Au wengine wanasubiri mpaka waulizwe wanataka nini, ndio wanasema. 
Sisemi kwamba uwe mkimya tu hata kama una shida ya kitu fulani na unafahamu kwamba ukimweleza mwenza wako anaweza kukusaidia, hapana! kama unaona kwamba uwezekano wa kupata kile ambacho unakihitaji upo mweleze kwa utaratibu naamini atakuelewa na kukutimizia.Tabia ambayo hawaipendi wanaume wengi ni ile ya kulazimisha ufanyiwe kitu fulani wakati inawezekana uwezekano haupo.
 
WAVUMILIVU
Wapo wanawake ambao sio wavumilivu kabisa katika maisha.Tunajua kwamba maisha siku zote hayatabiriki, yanaweza kutokea matatizo ya kiafya ama kifedha.Huu ndio wakati wa kuona uvumilivu wa mtu.Kama mwanamke anatarajia kwamba siku zote ni za raha tu na pindi matatizo yanapotokea anachukua uamuzi wa kumtoroka mwanume, huyo siyo mwanamke wa kuoa.
Wangapi leo hii huwatoroka waume zao pindi inapotea kuumwa, kufilisika ama kupatwa na tatizo lolote ambalo kwa namna moja ama nyingine yanaweza kuwafanya maisha yao kutingishika?
 
Uvumilivu kwa mwanamke utakuwepo kama tu atakuwa na mapenzi ya dhati kama nilivyozungumza hapo awali. Mwanamke mweye mapenzi ya dhati ni lazima atakuwa mvumilivu na atakuwa tayari kuishi katika maisha ya aina yoyote, yawe ya raha ama ya starehe.Hawa ndio wale ambao wanaume wengi wengependa kuwa nao maishani mwao.
 
Licha ya kupenda kuoa wanawake amabo wana tabia hizo nilizozitaja hapo juu, wanachukizwa sana na wanawake ambao wanavijitabia vidogo vidogo ambavyo kimsingi havikubaliki katka jamii.
Tabia hizo ni kama wambea, wasio wakweli na wawazi, wasioridhika, wagumu kusamehe na wapesi wa kuchukia, wagomvi na wenye roho ya kwanini.
 Utafiti huu umefanyikwa kwa baadhi ya wanaume ambao wanatarajia kuoa wanawake ambao wanaoishi katika maeneo mbalimbali jijini Dar-es-Salaam.

 Kwa maana hiyo basi hiyo iwe changamoto kwa wanawake. Wajue kwamba wanaume wanafurahi kuwa na wanawake wa aina gani. Hata kama utakuwa umeshaolewa, kama kuna wakati kunakuwa na kutokuelewana baina yenu, chunguza yawezekana kwamba unakosa mojawapo ya tabia ambazo nimezitaja hapo juu. Waweza kubadilika kwani inawezekana.

Wednesday, October 24, 2012

Mwanamke kuwa chini ya Mwanaume sio sababu ya kunyanyaswa




LIPO jambo gumu katika ulimwengu wa uhusiano ambalo limekuwa tatizo kubwa na fumbo linalowashinda wengi. Nazungumzia mwanamke kuwa chini ya utawala wa mwanaume. Kwa ujumla ni jambo la kawaida kabisa.

Huu ni msingi uliojengwa tangu zamani na hata kwenye mapitio ya vitabu vitakatifu yanaeleza juu ya jambo hilo. Kimsingi, hakuna tatizo katika nguvu hiyo ya mwanaume. Katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia, mambo yamebadilika kidogo na angalau mwanamke anapata nafasi mbalimbali kwenye jamii.

Wanawake wa leo wanapewa vipaumbe kwenye uongozi wa makampuni, taasisi, madhehebu ya dini, mashirika na vyama vya siasa na serikali. Pamoja na yote hayo, bado mwanamke anabaki kuwa mwenye wakati mgumu sana katika kufanya uamuzi au kujua hatma yake akiwa kwenye lindi la mapenzi.

Anaweza kuwa mwanamke bora, mwenye msimamo na tija kazini, lakini kwa mpenzi/mumewe anakuwa mpole asiyejua chochote kitakachokuwa mbele yake.

Ni eneo ambalo mwanamke anakuwa hana ujanja, hajiwezi na hajui cha kufanya, kwa sababu kila kitu kinachohusu uhusiano kwake kinakuwa na giza nene mbele yake. Huu ni ukweli.

Ni mada yenye ugumu kidogo kuingia akilini, lakini kichwa kikitulia na kupitia kwa umakini mkubwa, mstari kwa mstari unaweza kuelewa vyema na kubaki na kitu kipya kichwani mwako.
 
NI NINI HASA?
Ni kuwa chini ya mamlaka ya mwanaume. Kuwa chini ya matakwa na kufuata maelekezo. Wakati mwingine anaweza kupata nafasi ya kutoa mawazo yake, lakini ni juu ya maisha tu – si mustakabali wa mapenzi yao.

Mwanamke anaweza pia kutoa mapendekezo ya mapenzi yao, lakini hayawezi kuwa uamuzi. Hata kama akitoa uamuzi, bado siri ya uhusiano huo inabaki kuwa ya mwanaume. Mwanamke anaweza kuwa na upendo mkubwa, lakini akitegemea zaidi sapoti ya mwanaume wake.
Kwa maneno mengine, hata kama ana mapenzi yenye ukubwa gani, kama mwanaume wake atakuwa na uamuzi mwingine ambao yeye haujui, yote yanaweza kuwa kazi bure mwisho wa siku.
 
NI SAHIHI?
Hakika. Hakuna tatizo kwa mwanaume kuwa na mamlaka au uamuzi juu ya uhusiano wake. Si kwamba yeye ndiye aliyejipangia mwenyewe bali ni utaratibu alioukuta baada ya yeye kuzaliwa.
Mwanaume aliumbwa na kukabidhiiwa mamlaka moja kwa moja (mapitio ya vitabu Vitakatifu yanathibitisha hilo).   
 
KUNA ATHARI?
Ndiyo! Hapa ndipo kwenye msingi hasa wa mada yetu. Rafiki zangu, mamlaka ya mwanaume yamekuwa machozi kwa wanawake wengi. Kwa sababu wanawake hawana uwezo wa kujua kilichopo (hasa) ndani ya moyo wa mwanaume, wamekuwa wakitumia mawazo na fikra tu.
Mwanamke anaweza kuupumzisha moyo wake kwa mwanaume lakini akiwa hana uhakika wa nini kinachofuata, wakati mwanaume anaweza kumpenda mwanamke na kuendelea kubaki na siri yake ya nini kinachofuata ndani ya moyo wake.

Tunaona mengi kila siku kwenye jamii yetu. Mwanamke anafanya jambo kwa msingi wa kumfurahisha mpenzi wake, akiwa ameweka athari/mateso ambayo anaweza kuyapata kwa furaha ya muda kwa mpenzi wake.

Hata hivyo kipo kitu cha kufanya rafiki zangu. Kuwa chini ya himaya ya mwanaume hakukunyimi haki ya KUTAMBUA THAMA NI YAKO na NGUVU YA KUFIKIRI ILIYO NDANI YAKO. Bado mwanamke anaweza kuendelea kuwa mwenye mipango na kuamini kwamba nguvu ya ubongo wake ni kubwa kuliko hata mpenzi wake.

Kipo kitu cha kufanya, lakini ili kukufanya uelewe vizuri zaidi mada yenyewe, hebu twende tukaone matatizo wanayokutana nayo wanawake kutokana na kuacha nguvu ya MAMLAKA ya mwanaume ifanye kazi na kushindwa kutumia uwezo wa KUFIKIRI  uliopo ndani yao.
 
SUALA LA MIMBA
Kupata mimba kabla au nje ya ndoa ni tatizo. Ni jambo moja linalowahusu watu wawili lakini likiwa ndani ya uamuzi wa mwanamke. Mimba si bahati mbaya. Wanawake wanajua hili vizuri sana.
Wakati mwingine, wapenzi wanaweza kuwa wamepima ukimwi na hivyo wana uhuru wa kuamua kukutana kwa kutumia kinga au lah, lakini bado kuna suala la mimba ambalo linaweza kumgharimu mwanamke huyo.

Ukiacha hilo, inatokea mwanaume anamlazimisha mwanamke abebe mimba kwanza (eti) ndiyo atapeleka barua ya posa kwao. Inawezekana mwanaume huyo ana lengo hilo, lakini kwa nini alazimishe iwe kabla ya ndoa?

Kwa sababu sasa wanawake wengi huwa wanaacha nguvu yao ya kufikiri, wanajikuta wameingia mkenge! Mwisho jamaa anaingia mitini, mwanamke anabaki na mtoto wake.
Kwa nini uache hili litokee? Kwani hujui namna ya kujikinga na mimba? Ukiachana na kinga, kuna hata njia rahisi ya kuhesabu mzunguko wa mwezi, pia hujui? Nafasi yangu kwa leo imeisha. Hadi wiki ijayo kwa mwendelezo wake.
 
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani

Habari hii ni kwa hisani ya mtandao wa Global Publishers

Saturday, October 20, 2012

Faida na hasara ya Sweet, Baby.. kwenye Mapenzi


BABY ni neno la Kiingereza lenye maana ya mtoto, tena mara nyingi linatumika kwa mtoto mdogo. Pia lina maana nyingine ya mpenzi. Ni neno maarufu sana siku hizi; hata wazee kabisa, utasikia wanaitana baby!
Mbali na hilo, yapo maneno mengine kama sweet, dear, honey na mengine mengi. Maneno yote hayo ya Kiingereza, yana maana zaidi ya moja, lakini kubwa zaidi ni kumaanisha mpenzi, mpendwa (hutumika katika kuonesha mapenzi ya dhati kwa mwingine).
Leo nataka kukupa kitu kipya kabisa kichwani mwako. Unahitaji utulivu wa hali ya juu ili kujifunza hili. Ni maneno mazuri sana, ya kipekee lakini kwa upande mwingine ni hatari kwa sababu hukaribisha matatizo ambayo hayakutarajiwa na mtumiaji.
HUTUMIKA WAPI HASA?
“Dear, naomba uniamshe saa 12:00 asubuhi, kesho nina vikao vingi sana asubuhi,” inaweza kuwa kauli ya mume akimwambia mkewe, ambaye naye anamjibu: “Sawa sweet, usijali.”
Kwa hakika ndipo sehemu sahihi zaidi kutumika. Ni maneno yenye mshawasha mkubwa na huonesha penzi la dhati lililopo moyoni mwa mhusika kwenda kwa mpenzi wake.
Husisimua na kuongeza ladha ya mapenzi ya kweli. Kumuita mpenzi wako kwa majina ya kimapenzi huongeza zaidi upendo na msisimko wa moyo. Mwenzi hujiona wa kipekee na mapenzi huzidi kukua.
Kwa maana hiyo basi, ni sahihi zaidi kwa wapenzi kuitana majina niliyotaja hapo juu na mengine yanayofanana na hayo kwa lugha yoyote ile, ila iwe inatambulika vizuri na anayetamkiwa.
ATHARI SASA!
Kwa upande mwingine kuna athari za kutumia maneno hayo. Zama hizi, maneno hayo yanaonekana ya kawaida tu. Mtu yeyote anaweza kumuita yeyote mpenzi, honey, baby n.k. Hapo ndipo kwenye tatizo lenyewe.
Kwa ujumla wanawake ndiyo wanaongoza zaidi kuitana majina hayo. Wakati mwingine huenda mbali zaidi na kuwaita hata wanaume majina hayo ya kimapenzi. Si rahisi kuona athari zake kwa haraka na moja kwa moja, lakini zipo na wengi zimewasababishia matatizo. Ngoja tuone..
HUPUNGUZA THAMANI
Kama nilivyotangulia kusema awali, maneno
niliyotaja hapo juu husisimua na kuongeza mapenzi. Kwa kuyatumia vinginevyo, basi kwa kiasi kikubwa huanza kukuathiri na kupunguza thamani ya neno lenyewe.
Kama unaweza kumwita mfanyakazi mwenzako dear, mtu wa jinsi sawa na wewe sweet ni wazi hata utakapomuita mpenzi wako au wewe kuitwa na yeye, halitakuwa na nguvu sana ya mapenzi kwa sababu ni neno ulilolizoea kila wakati.
HUKARIBISHA USALITI
Wakati mwingine unaweza kujikuta umeingia kwenye usaliti bila kutarajia. Veronica, mfanyakazi wa saluni moja ya kiume iliyopo Sinza, Dar alitoa ushuhuda ufuatao:
“Mimi naishi na mchumba wangu, tuna mtoto mmoja mwenye miaka mitatu. Nafanya kazi saluni. Tangu nimeanza hii kazi, nimejifunza kutumia maneno matamu ya kumfurahisha mteja na wakati mwingine kumfanya akupe tipu baada ya kumaliza kazi.
“Kuna kaka mmoja nilizoeana naye sana. Kama kawaida, huwa namkaribisha kwa kumuita dear au sweet. Wakati nikiendelea kumfanyia scrub, mazungumzo yetu hutawaliwa na dear, sweet, nikajikuta nimezidi kumzoea.
“Kwa sababu tulibadilishana namba, mara akaanza kuwa na mazoea ya kunitumia meseji, akija ananipa pesa, anaondoka. Mazoea yakazidi. Nikajikuta nimemzoea na kuna siku ambayo siwezi kuisahau kabisa.
“Ni siku niliyomsaliti mchumba wangu...mbaya zaidi na huyo jamaa naye ana mke wake. Niliumia sana, lakini naamini kama nisingekuwa na mazoea ya kumuita majina ya kimapenzi nadhani nisingeingia mtegoni. Moyo wangu unauma sana, najuta kumsaliti mpenzi wangu.”
Unaweza usione athari hii moja kwa moja, lakini ndugu zangu chukua jambo hili leo; wanaume wengi wakiitwa kwa majina ya kimapenzi husisimka sana – hujiona wenye bahati na mara hushawishika kuingia mapenzi.
Kama mwanamke hatakuwa makini atajikuta ametumbukia. Ya nini yote hayo, wakati unaweza kubadilisha mazoea hayo?
ANGALIA TOFAUTI
Rafiki zangu, kati ya maneno niliyoyataja, kuna ambayo yanakubalika kutumiwa na wasio na uhusiano lakini wawe na undugu wa damu. Mathalani baba, mama, kaka, dada, shangazi nk.
Hakuna tatizo kumuita mtu mpendwa, lakini siyo baby, sweet, mpenzi na mengine yenye maana ya moja kwa moja ya kimapenzi. Umenipata? Akili za kuambiwa, changanya na zako kisha unazifanyia kazi! Chukua kinachokufaa!

Habari hii ni kwa hisani ya mtandao wa Global Publishers